Kutenda Dhambi Bila Kuvunja Sheria? | Maswali na Majibu | Pr Enos Mwakalindile

preview_player
Показать описание
Tafsiri ya dhambi kama uvunjifu wa sheria iko wazi. Yohana ashuhudia kuwa “kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi [uasi wa sharia, anomia]” (1Yoh 3:4). Paulo aungana naye akisema, “dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria” (War 5:13). Kwa kuwa ndivyo ilivyo, yawezekanaje kutenda dhambi bila kuvunja sheria?

Katika Warumi 2:12 Paulo anashuhudia kwamba, “wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria.” Ni makundi gani haya anayoyazungumzia? Unapomsikiliza Paulo kabla na baada ya hapa utatambua anazungumzia Wayahudi na Wasiowayahudi (Wamataifa).

Tukianza na kundi la kwanza. Wayahudi ndio waliiokadhibiwa “mausia ya Mungu;” hao ndio wenye “kuitegemea torati na kujisifu katika Mungu na kuyajua mapenzi yake” (War 3:2; 2:17, 18). Elimu ya Sheria (torati) ilikuwa kiongozi wa kuwaongoza kuwaleta kwa Mkombozi (Wagalatia 3:24); kumbuka, elimu ya torati haikuwa wokovu wenyewe bali iliwaandaa Wayahudi kupokea wokovu. Iliwaandaje? “Kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria” (War 3:20). Sheria iliwapa “waijuayo sheria” uzoefu wa namna dhambi inavyowashikiria wenye mwili na wana-Adamu hatiani na utumwani na mautini kiasi cha kutambulisha uhitaji wao wa kukombolewa (Angalia Warumi 7).

Tukija kwa kundi la pili. Wamataifa hawakupewa torati kama Israeli ilivyopewa kwa mkono wa Musa. Je! wao kutopewa sheria, kutopewa elimu inayoainishia hatia na uweza na matokeo ya dhambi, kunawafanya wapotee chini ya dhambi na nje ya familia ya Ibrahimu? Wamataifa, wanaojulikana si wana wa Ibrahimu kwa kutotahiriwa kwao, wanapotenda sawa sawa na elimu ya sheria, hawafanani na wana wa Ibrahimu waliotahiriwa na wenye elimu ya torati? “Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutokutahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa?” (War 2:26, angalia pia 28-29).

Dhambi inaenda mbali zaidi ya uvunjifu wa torati. Kwa Myahudi kwenda kinyume na tohara ya Musa, kwenda tofauti na sheria iliyoainisha nani ni wana wa Ibrahimu kwa jinsi ya kimwili kulihesabika kuwa dhambi mpaka Yesu aliyekusudiwa na torati alipokwea msalabani na kutoa si govi tu bali mwili wote kama tohara kamili na utambulisho kamili kwa Wayahudi na Wasiowayahudi wanaomwamini. Anayeyashika maagizo ya torati ni muumini yeyote, Myahudi aliyetahiriwa na Mmataifa asiyetahiriwa, anayemtambua Yesu Mkombozi kama tohara yake kama utambulisho wake wa moyoni, kama torati ilivyoagiza, ilivyoelekeza kwake.

Kwa Wamataifa ambao hawakuwa chini ya torati iliyowaelekeza Wayahudi kwa Yesu, kwa wasiotahiriwa waliomwamini Yesu na kumchukulia Yeye kama tohara yao, kama utambulisho wao, Imani ndiyo mwamuzi haki.

Muumini anaweza kutenda dhambi bila kuvunja sheria pale anapokwenda kinyume na Imani yake katika Yesu Masihi. Warumi walipokuwa wakhukumiana kwa habari za vyakula na sikukuu za ibaada kwa mujibu wa sheria, Paulo akawakumbusha wao ni wa Masihi na matendo yao hayanabudi kupelekana na Imani (uaminifu, pistis, ya Yesu). Akasema, “kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi” (War 14:23)

Muumini anaweza kumpendeza Mungu hata bila ya uwepo wa sheria. Hata kabla torati ya Musa haijakuwepo Ibrahimu baba wa Imani alimpendeza Mungu. “Akiiona ahadi ya Mungu [kuumpa familia] hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu” (War 4:20). Watoto wa Ibrahimu wanaweza kufuata nyayo za baba yao kwa kuzingatia agizo hili. “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu” (1 Wakorintho 10:31).

Yawezekana muumini asiyetahiriwa, mmataifa aliyemwamini Yesu Kristo, asiwe amekwenda kinyume na sheria yoyote iliyoandikwa kitabuni, Bibliani, lakini akawa amekwenda kinyume na Mungu aliyetukuzwa na uaminifu wa Yesu. Hapo atakuwa ametenda dhambi, amepungukiwa na utukufu wa Mungu uliofunuliwa katika uaminifu wa Masihi. Roho Mtakatifu anamfunulia muumini yeyote utukufu, uaminifu wa Mungu Baba kwa watu wake kama ulivyotabiriwa na manabii na kama ulivyofunuliwa na Mwanawe. Lengo ni kwamba tuuakisi upendo wa Baba unaojulikana ndani ya mwanawe, ufunuo hata ufunuo, utukufu hata utukufu. Tofauti na utukufu wa Mungu ni dhambi, ni upungufu wa utukufu tuliofunuliwa tuurithi ndani ya Masihi, ni uasi kwa imani iliyoshuhudiwa na Musa na manabii.

Yatosha tuseme hivi, haiwezekani kutenda dhambi bila kwenda kinyume na Imani; japokuwa yawezekana kutenda dhambi bila kuvunja sheria.

Swali: unajisikia binadamu zaidi pale unapoishi kwa kufuata sheria bila kumjua Mungu au unapomjua Mungu na kufuata maagizo yake?

Una maoni? Tunatamani kukusikiliza. Acha maoni yako hapa chini.

Una hitaji kukutana na Pr Enos Mwakalindile kwa ushauri au maombi? Tuma ujumbe mfupi kwa simu namba: +255656588717 (WhatsApp)

Рекомендации по теме